Viongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wameaswa kuongeza zaidi tafiti na uzalishaji wa mbegu za asili na kujenga uwezo wa watafiti wake kupitia vyuo vya ndani na nje ya nchi.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amemweleza hayo Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana wakati wa ziara yake katika Kituo cha Utafiti cha TARI – Naliendele, mkoani Mtwara Septemba 30, 2024.
“Naelekeza pia nyaraka za kuanzisha mfuko wa kufanya tafiti za kilimo ‘agricultural research fund’ na kanuni zake ziandaliwe ili kuiwezesha TARI kutunza rasilimali fedha zitakazotokana na makato ya mazao kwa lengo la kuwezesha uendelezaji wa tafiti za kilimo nchini,” amesema Waziri Bashe.
Aidha, Waziri Bashe ametolea mfano wa makusanyo yanayotokana na makato kwenye mauzo ya zao la korosho ambapo kwa mikoa ya Mtwara na Lindi ni shilingi 25 kwa kila kilo, huku zao la ufuta ni shilingi moja hadi mbili kwa kilo kwa mikoa hiyo.
“Mfuko wa ‘agricultural research fund’ ukishapatikana, tutaweka utaratibu kwa mazao mengine ili makusanyo hayo yaweze kuendesha shughuli mbalimbali kama vile tafiti au kujenga uwezo kwa watafiti,” amesema Waziri Bashe.
Kwa upande wa uzalishaji wa mbegu (seed multiplication), Waziri Bashe ameelekeza wataalamu waanze kuainisha mbegu tofauti (characterization) kwa kila zao (kama vile za asili, za kisasa, organic, hybrid, n.k.) ili kumwezesha mkulima akienda dukani awe na nafasi ya kuchagua aina ya mbegu anayoitaka kutoka kwenye aina mbalimbali za mbegu ya zao moja.
Wataalamu wa TARI wameeleza kugundua aina za mbegu bora 64 za zao la korosho, ambalo ni zao linalokabiliwa na visumbufu vya wadudu aina mbalimbali wakiwemo Ubwiriunga, Dieback, Mbu wa Mikorosho, Vidung’ata, Vithiripipi au Kifauwongo.
Aidha, imeelezwa kuwa kuna aina 8 za mbegu bora mpya (TARIKO 1-8) za korosho zenye uwezo wa kukabiliana na magonjwa visumbufu ya “blaiti” na mnyauko fusari.
Wakati wa ziara hiyo, Waziri Bashe amekagua Kituo na kupata taarifa kutoka kwa watafiti kuhusu tafiti za mbegu za korosho, ufuta, karanga, njugu na mboga mboga.