Serikali kupitia Maonesho ya Swahili International Tourism Expo- SITE imezidi kufungua milango ya fursa katika sekta ya utalii zinazopatikana nchini kwa wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana Oktoba 14, 2024 Jijini Dar es Salaam, alipofunga rasmi Onesho la Kimataifa la Utalii la Swahili International Tourism Expo ambalo limedumu kwa siku ya tatu.
Waziri Chana amesema kuwa Onesho hilo ni matokeo chanya ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika jitihada zake za kuibua fursa kwenye sekta ya utalii nchini ili Watanzania waweze kuzichangamkia kwa lengo la kuboresha maisha yao na kuinua uchumi wa nchini.
Chana amewapongeza wadau wote wa Utalii walioshiriki katika maonesho hayo na kuahidi kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii nchini itaendelea kushirikiana vyema na wadau wote wa ndani na nje katika kuhakikisha sekta ya Utalii inakuwa zaidi kwa maslahi mapana ya Taifa.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Utalii Tanzania, Balozi Dkt. Ramadhan Dau, ameushukuru uongozi wa Wizara kwa kazi kubwa inayofanya ya kukuza na kuendeleza Utalii nchini na kwamba TTB itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kutangaza Utalii ndani na nje ya nchi.
Akizungumza kwa niaba ya wanunuzi wa bidhaa za Utalii waliohudhuria Onesho hilo, Reno Mauricio kutoka nchini Ureno ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa mazingira mazuri ya uwekezaji iliyoweka kwa wadau wa utalii kutoka nje ya Tanzania hali inayopelekea wengi kuchangamkia fursa zilizopo nchini.
Maonesho hayo Makubwa ya utalii, yamewakutanisha wanunuzi wa bidhaa ya utalii zaidi 120 na nchi washiriki takribani 50 yalifunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussen Ali Mwinyi.