Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amewataka Viongozi na Watendaji wa SACCOS nchini kuendelea kubuni bidhaa na huduma zinazoendana na mahitaji ya wanachama pamoja na kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa wanachama na Watanzania ili kuongeza matumizi ya huduma za fedha nchini.
Amesema hayo Oktoba 21, 2024 wakati akifungua Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo (ICUD 2024) zinazofanyika katika viwanja vya Mirongo Jijini Mwanza.
Ameeleza kuwa kazi zinazofanywa na Ushirika wa akiba na mikopo zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa kwenye shughuli za kiuchumi na kijamii.
“Ni nia yetu ya dhati kabisa kama wasimamizi wa Sekta hii ya Ushirika nchini kuhakikisha mazingira ya kiuendeshaji kwa SACCOS yanaendelea kuboreshwa na kuwa salama wakati wote. Tunathamini sana mchango wa SACCOS kwenye utoaji wa huduma jumuishi za kifedha,” amesema Silinde.
Pia, Silinde ametaka wanaushirika nchini kuendelea kutumia mfumo wa MUVU katika uendeshaji na usimamizi wa Shughuli za Vyama vya Ushirika ikiwemo SACCOS pamoja na matumizi ya TEHAMA kwa kutumia mifumo mbalimbali iliyopo sokoni inayoendana na uwezo wa Kifedha ikiwemo mfumo ulioandaliwa na unaondeshwa na Muungano wao (SCCULT) ili kuwahudia wanachama vizuri na kuhimili ushindani uliopo kwenye soko la fedha.
Naye Mrajis na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, ameeleza Tume imepokea maombi 1,211 ya Leseni kutoka kwa SACCOS na ilikuwa imetoa Leseni 963 kwa SACCOS zilizokidhi sifa na vigezo vya kupewa Leseni hizo kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha.