Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Tanzania kuandaa World Travel Awards 2025: Dkt Abbasi

Tanzania kuandaa World Travel Awards 2025: Dkt Abbasi

0 comment 9 views

Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema Tanzania inakwenda kuandaa Tuzo za Utalii duniani (World Travel Awards, WTA) kwa Bara la Afrika kwa mwaka 2025.

Dkt. Abbasi amesema hayo Novemba 26, 2024 wakati akiongea na vyombo vya habari mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam kutoka nchini Ureno ambapo Tanzania ilitwaa Tuzo ya Dunia ya Sehemu Maridhawa Zaidi kwa Utalii wa Safari 2024 (World’s Leading Safari Destination).

Dkt. Abbasi amefafanua kuwa Tanzania imepata Tuzo hiyo kutokana na ushirikiano mkubwa wa wadau mbalimbali wa Utalii nchini katika kutangaza vivutio vya utalii.

Aidha, amesema kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuitangaza Tanzania kupitia Filamu ya The Royal Tour na Amazing Tanzania imesaidia kuitangaza Tanzania kimataifa.

Soma: Tanzania ndio eneo maridhawa zaidi kwa utalii wa safari duniani

Soma: Rais Samia aahidi kufanya “Royal Tour” kuitangaza hifadhi ya Katavi 

Ameongeza kuwa Tuzo hizo ni ishara ya kwamba wageni wamekuwa na imani kubwa na vivutio vya utalii na ukarimu ambao wamekuwa wakipata wakati wanapokuja kutembelea vivutio hivyo na kuwataka kuendelea kuwa wakarimu.

Ametoa wito kwa watanzania wote kushirikiana na Serikali katika kulinda na kuhifadhi vivutio vya utalii na raslimali zilizopo ili viweze kuchangia kwenye uchumi wa taifa.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Ephraim Mafuru amesisitiza kuwa kwa sasa Tanzania inakwenda kutangaza mazao mapya ya utalii ili kupanua wigo wa vivutio vya utalii na hivyo kuwafanya wageni kuongeza siku za kukaa na kutumia wakifika nchini.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dkt. Thereza Mugobi amesisitiza wadau wote nchini kuzingatia sera na kanuni mbalimbali zilizowekwa na Serikali ili sekta ya utalii nchini iendelee kukua.

Soma: Royal Tour yaongeza mapato kutoka Tsh 70bn hadi Tsh 84bn

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter