Wananchi wametakiwa kubainisha matumizi yasiyo ya lazima na kuyaondoa na kufanya kuweka akiba kuwa ni sehemu ya lazima kila wanapopata fedha.
Aidha, Afisa Mwandamizi Masoko na Mawasiliano kutoka Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, ametoa wito kwenye semina zinatolewa na Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha ilifanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, na kwa Wanavikundi na Wajasiriamali wadogo wadogo ilifanyika katika Ukumbi wa Family Conference Hall na Ofisi ya Tarafa ya Siha Kati, Kata ya Fuka mkoani Kilimanjaro.
Mwanga amewahimiza watumishi wa umma, wanavikundi na wajasiriamali wadogo wadogo kujijengea utamaduni wa kuweka akiba kila wanapopata kipato ili iwasaidie kuwaongezea katika uwekezaji na kukuza uchumi.
“Ili kuweka akiba ya fedha ni vyema ukaondoa matumizi yasiyo ya lazima na kujifunza kuweka akiba kila unapopata fedha,” amesisitiza Mwanga.
Katika semina hizo, watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, wanavikundi na wajasiriamali wadogo wadogo wamejengewa uelewa wa elimu ya fedha.
Akiikaribisha Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Haji Mnasi, alisema kuwa amefurahishwa na ujio wa Timu hiyo kuja kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya uwekaji akiba, mikopo na uwekezaji kwani ni fursa kubwa kwa watumishi wa Halmashauri yake.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Salim Kimaro alisema ni vyema watumishi wa umma wakatumia elimu hiyo ya fedha ili kuboresha matumizi yao ya kila siku na kuweka akiba ili kuepuka kuchukua mikopo kausha damu.
“Elimu hii itawawezesha kufahamu ni wakati gani unatakiwa kuchukua mkopo na namna bora ya kuutumia, pia itawawezesha kufahamu mahali salama kwa kuwekeza fedha kidogo kidogo ili kuboresha hali ya uchumi na kuwaondolea mawazo ya kukopa kila wakati,” alisema Kimaro.