Gavana wa Benki Kuu ya (Tanzania BoT) Emmanuel Tutuba, amesema utafiti wa Finscope wa mwaka 2023, unaonesha kuwa wanawake hawajafikiwa na wana matumizi madogo ya huduma rasmi za kifedha.
Gavana Tutuba amesema hayo Machi 05, 2025 kwenye mkutano na viongozi mbalimbali wa sekta ya fedha, hususan sekta ya kibenki, pamoja na wadau wa maendeleo.
Katika mkutano huo, wamejadili masuala mbalimbali yatakayosaidia kuziba pengo la kijinsia katika Huduma Jumuishi za Fedha nchini.
Ameongeza kuwa mkutano huo utajadili fursa zilizopo na namna ya kutumia fursa hizo katika kuziba pengo lililopo kati ya wanaume na wanawake katika upatikanaji na utumiaji wa huduma za fedha nchini.
Aidha, amesisitiza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayoandaliwa kwa upande wa Tanzania Bara, zinatazamia kuwa na uwiano wa asilimia hamsini (50) kwa hamsini (50) kati ya wanawake na wanaume ifikapo 2033.
Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Theobald Sabi, amesisitiza kuwa benki zinaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuwafikia wanawake wengi na biashara zinazomilikiwa na kundi hilo ili kufikia lengo la uwiano wa asilimia 50 kwa 50 kati ya wanaume na wanawake.
Amesema hatua hizo ni pamoja na ubunifu unaofanywa na benki za biashara katika kutengeneza bidhaa na huduma za kibenki mahususi kwa ajili ya wanawake ili kuondoa madhila mbalimbali yanayowakumba ikiwemo ukosefu wa mikopo.
Kwa upande wake, Meneja wa Taasisi ya Fedha ya Kimataifa (IFC) kwa nchi za Tanzania, Rwanda na Uganda Martine Valcin amesema suala la ujumuishi wa kijinsia katika upatikanaji na utumiaji wa huduma rasmi za kifedha ni la kipaumbele kwa Benki ya Dunia kutokana na mchango wake katika kustawisha uchumi wa Tanzania na dunia kwa ujumla.
Wendy Teleki, ambae ni kiongozi wa Mpango wa Kuwawezesha Wajasiriamali Wanawake (WE-FI) ameeleza kuwa Makubaliano ya Mpango wa Kuwawezesha Wajasiriamali Wanawake (Women Entrepreneurs Finance Initiative Code) uliozinduliwa katika mkutano hou unalenga kuzikutanisha taasisi za fedha ili kuingia kwenye makubaliano ya kuwawezesha kifedha wajasiriamali wanawake.