Home VIWANDANISHATI Tanzania yang’ara utekelezaji shughuli za uwazi na uwajibikaji sekta ya madini

Tanzania yang’ara utekelezaji shughuli za uwazi na uwajibikaji sekta ya madini

0 comment 11 views

Serikali imesema itaendelea kuweka wazi taarifa za uwekezaji na mapato yanayopatikana katika sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia nchini kama Sheria inavyotaka na kwa kuzingatia vigezo vya Uwazi na Uwajibikaji vinavyosimamiwa na Asasi ya Kimataifa ya EITI.

Hayo yameelezwa Machi 13, 2025 na Innocent Bashungwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati akifungua mkutano wa 62 wa bodi ya Kimataifa ya Uwazi na Uwajibikaji (EITI) jijini Arusha.

Waziri Bashungwa amesema wananchi wanapaswa kufuatilia na kujua mambo yanayoendelea katika sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa mapato hayo yanawekwa wazi kwa lengo la kuimarisha uaminifu kwa wananchi.

Aidha, Waziri Bashungwa amesema “kwa kuzingatia Tanzania ni mwanachama wa bodi ya EITI inayosimamia Uwazi na Uwajibikaji, Mwaka 2015 Serikali ilitunga Sheria ya kusimamia Uwazi na Uwajibikaji katika rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia, sura 447.”

Kwa upande wa Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema Taasisi ya TEITI inayosimamia Uwazi na Uwajibikaji nchini, imekuwa ikifanya vizuri kazi yake ambapo taarifa ya mwisho imeonyesha Serikali imeendelea kufanya vizuri katika kuweka Uwazi na Uwajibikaji wa taarifa za mapato yanayopatikana katika sekta hizo.

“Watu wengi wamekuwa wakitamani kuona nchi yetu inanufaikaje na rasilimali zilizopo kwenye Madini, Mafuta na Gesi Asilia, kwa kupitia utaratibu huu wa Uwazi na Uwajibikaji ambao unawekwa kwenye taarifa za mapato ndipo wananchi wetu wanaweza kufahamu jinsi rasilimali hizo zinavyoweza kututajirisha, ” amesema.

Amesema chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia zimekuwa zikifanya vizuri na hivyo kuvutia wawekezaji wengi zaidi Nchini.

Pamoja na hayo,  Waziri Mavunde ameeleza kuwa kufanyika kwa mkutano wa 62 wa Bodi ya Kimataifa – EITI hapa nchini ni matokeo mazuri ya Tathmini ya EITI iliyofanyika mwaka 2023.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter