Watu wengi wanahitaji mikopo ili kujiendeleza katika shughuli zao mbalimbali za maendeleo. Kama wewe ni mfanyabiashara mdogo bila shaka unatamani kupata mkopo ili kuongeza mtaji wako ambao utapelekea ubora zaidi katika bidhaa au huduma inayotolewa. Lakini ikitokea unapata mikopo hii unaitumiaje? Matumizi yako ya fedha hizi yanakuhakikishia upatikanaji wa fedha zaidi? Ni vitu gani hutakiwi kufanya pindi unapopata mkopo? Makala hii inalenga kuelezea machache ambayo hayashauriwi kufanywa pale unapofanikiwa kupata mkopo.
Kwanza kabisa usikope ili kuanza biashara. Hili ni kosa kubwa ambalo watu wengi hufanya. Hutakiwi kuanza biashara na fedha ya mkopo kwani huna uhakika wowote kama biashara yako itarudisha faida katika kipindi cha mwanzo. Ni vizuri kupambana mpaka unzishe biashara yako, isimame na kuonyesha matumaini kidogo hapo ndipo unaweza kuhangaikia masuala ya mkopo ili ukusaidie kuboresha huduma zako. Wengi ambao wanaanzisha biashara kwa mikopo hawafanikiwi.
Usichukue mkopo ili kufanya matumizi binafsi. Watu wengi huona muda waliopewa na taasisi za kifedha ili kurejesha mikopo ni mrefu hivyo hujisahau na kutumia fedha hizo katika matumizi binafsi ambalo hayana faida kiuchumi. Fedha za mkopo zinatakiwa kuwekezwa pale ambapo unaona kuna muelekeo wa fedha hizo kurejeshwa au zitumike katika shughuli za kiuchumi ambazo zinamuhakikishia mkopaji kipato zaidi. Kutumia fedha za mikopo katika matumizi binafsi sio busara kwani hutakuwa umeziweka katika shughuli yoyote ya kimaendeleo.
Pia wakati unafikiria kuomba mkopo ni vizuri kuchukua mkopo ambao una uhakika utaweza kuurejesha ndani ya muda uliopangwa. Usiombe mkopo mkubwa ambao utakupa matatizo wakati wa kurejesha. Ni vizuri kuchukua mkopo ambao upo ndani ya uwezo wako ili usijiweke katika hali ya kupoteza biashara yako au hata mali zako binafsi pale utakaposhindwa kuurudisha. Unatakiwa kukopa fedha ambazo zipo ndani ya uwezo wako kuzirudisha hata kama mipango yako haitaenda kama ulivyotarajia.
Hakikisha unatumia fedha za mkopo kama ulivyopangilia. Kabla ya kuomba mkopo ni vizuri kuandaa mpango wako wa biashara na kuandika matarajio yako yote ili iwe rahisi wakati ukishapata mkopo. Ni vizuri kujiwekea malengo na kuwa na mikakati ya jinsi ya kutumia mkopo vizuri ili ufaidike nao na pia ufanye marejesho kwa wakati, hali ambayo itafanya taasisi husika kukuamini na kujenga mahusiano ya muda mrefu.