Rais John Magufuli ameiagiza Benki ya NMB kuongeza gawio linalotolewa kwa serikali kwani japokuwa benki hiyo inatengeneza faida kila mwaka, serikali ambayo ni mbia wake kwa asilimia 32 haijapata ongezeko lolote katika gawio lake kwa takribani miaka mitatu. Rais Magufuli amesema hayo kabla ya zoezi la kufungua jengo la PSPF na tawi la Makao Makuu ya Benki ya NMB mjini Dodoma jana.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Rais ameeleza kuwa mwaka 2012/13, NMB ilitoa gawio la Sh. 10.8 bilioni, mwaka 2013/14 ilitoa Sh. 14.301 bilioni na kuanzia mwaka 2014/15 hadi 2016/17 walitoa Sh. 16.525 bilioni, kiwango ambacho hakijabadilika kwa miaka mitatu.
Mbali na agizo hilo, Rais Magufuli ametoa pengezi kwa benki hiyo kwa kufikia takribani asilimia 98 za wilaya kutokana na uwepo wa matawi 250 ya benki hiyo vijijini, ATM 800 na wakala 600,000. Vilevile amepongeza benki ya NMB kwa kutumia kiasi cha Sh. 1.4 bilioni kwa ajili ya kusaidia huduma mbalimbali katika jamii ikiwemo kutoa kompyuta 300 pamoja na kutengeneza madawati 6,000.