Home VIWANDAMIUNDOMBINU Kitendawili cha miundombinu vijijini mpaka lini?

Kitendawili cha miundombinu vijijini mpaka lini?

0 comment 99 views

Na Mwandishi Wetu

Kuwa na miundombinu bora kunasaidia sana katika kurahisisha shughuli za kimaendeleo. Bila kuwa nayo, mazingira yanakuwa magumu katika harakati mbalimbali za kiuchumi. Serikali imekuwa ikiongeza jitihada zake kuhakikisha kuwa huduma mbalimbali zinaboreshwa hapa nchini hasa vijijini ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaondokana na kero ambazo zinapelekea kuzorota kwa maendeleo katika jamii hizo.

Mojawapo ya kero hizi ni ubovu wa barabara. Kuwepo kwa barabara ambazo hazina ubora na hivyo kufanya usafiri kuwa wa shida na gharama unarudisha nyuma maendeleo kwa kiasi kikubwa. Hakuna walimu wanaotaka kwenda kufundisha katika sehemu hizi hivyo jamii hizi hubaki bila elimu bora. Kwa upande wa wataalamu pia, shughuli mbalimbali za kiuchumi zinakwama kutokana na kero ya usafiri hivyo wataalamu hawa hubaki mijini tu wakiacha huduma hizi vijijini kuzidi kuwa mbaya.

Mawasiliano nayo ni sehemu kubwa ya maendeleo. Huduma za simu zilizopo mijini zinapelekea shughuli mbalimbali za biashara kufanyika. Lakini hali hii haipo katika vijiji ambavyo makampuni haya yameshindwa kuweka minara na kuwapatia wananchi hawa huduma ya mawasiliano. Jambo hili linapelekea wafanyabiashara vijijini kuwafikia watu wa karibu yao pekee. Lakini fikiria, kama wasingekuwa na changamoto ya mawasiliano wangehudumia watu wangapi zaidi? Huduma hizi zingewapatia wateja wangapi wapya? Huduma wanazotoa zingewafikia wangapi kwa urahisi zaidi?

Umeme nao ni changamoto kubwa vijijini. Ukosefu wa nishati hii unawarudisha nyuma waishiyo vijijini kwa kiasi kikubwa kwani bila umeme shughuli nyingi za kimaendeleo haziwezi kufanyika. Vijiji vingi kukosa nishati hii muhimu kunafukuza wawekezaji katika maeneo hayo, uwekezaji ambao ungeweza kuanzisha viwanda na hivyo kuzalisha ajira kwa wazawa hawa. Serikali imekuwa ikifanya michakato kuhakikisha kuwa hakuna sehemu itakayokuwa bila umeme hapa nchini hivyo hilo linawapa tumaini jipya wakazi hawa kuwa hivi karibuni nao hawataachwa nyuma.

Wakazi wengi wa vijijini hujihusisha na shughuli za kilimo lakini ni wachache sana wanaofanya kilimo ambacho kinawaletea manufaa. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya kilimo wanatakiwa kusaidia jamii hizi na kuwaelimisha juu ya mbinu bora zaidi ya kilimo ili wapate kuzalisha kwa tija na kunufaika na kile ambacho wanafanya. Kuwapelekea miundombinu bora ni njia mojawapo ya kuwasaidia wakulima katika shughuli zao.

Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa tunachangia katika kuinua pato la taifa na kujikomboa na umasikini lakini lengo hilo haliwezi kufikiwa kama hakuna mifumo bora ambayo kwa namna moja ama nyingine itasaidia katika kurahisisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo. Hivyo miundombinu inapaswa kuboreshwa ili kuwapa wananchi nguvu zaidi katika kuipeleka nchi yetu kwenye mafanikio.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter