Home BIASHARAUWEKEZAJI Serikali iimarishe ngazi hizi muhimu za maendeleo

Serikali iimarishe ngazi hizi muhimu za maendeleo

0 comment 94 views

Hakuna anayependa kukwama kiuchumi na kubaki katika dimbwi la umaskini. Watanzania wengi ni wachapakazi lakini hawawezi kwenda popote bila uongozi uliopo madarakani kuwapa motisha na kurahisisha njia kwa mtanzania wa kawaida. Wananchi watashindwa kuwa katika nafasi bora zaidi kiuchumi endapo serikali haitachukua hatua katika sekta muhimu ambazo haziepukiki katika shughuli za kiuchumi hasa kwa wananchi wanaoishi vijijini.

Sekta ya kwanza muhimu ni elimu. Hakuna nchi yenye maendeleo bila mfumo bora wa elimu. Shughuli yoyote yenye kuleta maendeleo lazima iende sambamba na elimu bora. Kuna haja ya serikali yetu kuhakikisha vijijini kuna walimu waliofuzu na wanaojitosheleza. Shule zinapaswa kuwa na majengo ya kutosha pamoja na vitabu, maabara na mazingira salama ambayo yatapelekea mwanafunzi kuzingatia elimu tu na siyo vinginevyo.

Katika sekta hii pia, elimu ya ujasiriamali inatakiwa kuanza kutolewa tangu ngazi ya chini. Tatizo la ajira limezidi kukithiri nchini hapa kwa sababu hatujui la kufanya pindi tunapokosa kazi baada ya kumaliza masomo.

Miundombinu pia inapaswa kuboreshwa ili kuwezesha shughuli za kibiashara kufanyika sehemu kutoka sehemu moja au nyingine. Barabara zenye viwango zijengwe kwa wingi vijijini, vivuko navyo vijitosheleze na serikali iangalie uwezekano wa kutoa kodi zisizo na ulazima hapa nchini ili mfanyabiashara apate faida zaidi kutokana na kile anachokifanya. Biashara hutegemea sana miundombinu hivyo bila kuwa na ubora wa hali ya juu katika sekta hii, shughuli mbalimbali za kiuchumi nazo zinakwama.

Kama ambavyo ni azma ya serikali kujenga Tanzania ya viwanda, ni muhimu kwa serikali hiyo hiyo kwanza kuinoa sekta ya kilimo. Bila wakulima hapa nchini malighafi zote zinazohitajika ili kujenga Tanzania ya viwanda zitapatikana wapi? Hivyo viongozi wanapaswa kuwa bega kwa bega na kuwaondolea chanagamoto wakulima hapa nchini kusudi malengo yao ya kila msimu yafikiwe.

Hali ya masoko nayo pia iwekewe mkazo. Ili kusaidia wakulima kuuza bidhaa zao na kunufaika na kilimo wanachofanya, ni vizuri kuwepo na soko la uhakika hapa ndani na nje kwa ujumla. Vyama vya ushirika visimamiwe kwa ukaribu zaidi kwani wakulima wengi wanavitegemea. Vitendo vya uongozi mbovu katika taasisi muhimu kama hizi katika maendeleo ya kilimo visiwe vya kufumbia macho.

Serikali ikiboresha sekta hizi, wananchi nao wanafarajika na kupata nguvu zaidi wakiwa wanatekeleza wajibu wao wa kujenga taifa. Serikali kupitia wizara zake mbalimbali inapaswa kuwa sikivu na kuelewa wananchi wake hivyo kujua jinsi gani ya kuwawekea mazingira bora kiuchumi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter