Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa siku sitini (60) kwa wamiliki wa viwanja visivyoendelezwa kujitathmini juu ya kuviendeleza viwanja hivyo. Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dorothy Mwanyika amesema hayo na kusisitiza kuwa endapo wamiliki hao wasipochukua hatua stahiki, wapo katika hatari ya kubadilishwa umiliki kwa mujibu wa sheria.
Kati ya mwaka 2001-2008, takribani viwanja 40,000 viliuzwa kwa watu binafsi, taasisi na makampuni mbalimbali lakini mpaka sasa asilimia kubwa ya viwanja hivyo havijaendelezwa.
Akihusianisha kifungu cha sheria namba 42(2) cha Sheria ya Ardhi (Sura 113) kinachompa Rais mamlaka ya kuondoa umiliki wa ardhi kwa mtu aliyeshindwa kuendeleza kiwanja chake kwa zaidi ya miaka miwili, Mwanyika chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi amesema kwa kushirikiana na serikali za mitaa wameanza kufanya ukaguzi wa viwanja hivyo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es salaam.