Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ametoa maagizo kwa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji (PIC) kutafiti chanzo cha Benki ya NBC kulipa gawio kidogo kwa serikali ikilinganishwa na benki nyingine. Ndugai ametoa agizo hilo wakati akifungua semina ya siku moja kwa kamati hiyo na viongozi wa NBC.
Spika ameonyesha kushtushwa na taarifa zilizotolewa kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu benki ya NBC ilitoa kiasi cha bilioni moja pekee kama gawio. Amehoji kwanini kiasi hicho kipo chini kuliko benki nyingine ikiwa serikali ina hisa asilimia 30 katika taasisi hiyo.
Aidha Ndugai amedai benki hiyo inadhihirisha kutokuwa na urafiki na wananchi kutokana na kutokuwa karibu nao kwa kushindwa kufungua matawi na pia kutotoa mikopo kwa wananchi waliopo kijijini kama benki nyingine zinavyofanya.
Spika Ndugai amehitimisha kwa kuagiza PIC kuyapitia mashirika yake 272 ya umma ambayo serikali ina hisa ili kujua maendeleo yake lakini pia kupitia mashirika ambayo serikali inataka kuingia mikataba nayo ili kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza siku za usoni.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa kamati ya PIC, Raphael Chegeni ametoa wito kwa benki ya NBC kuamka na kuongeza nguvu katika utoaji huduma kwani kipindi hiki ni kipindi cha ushindani. Naye Kaimu Mkurugenzi wa NBC Theobald Sabi amesema hivi sasa wanasonga mbele wakiendelea kuikuza benki hiyo ambayo hivi sasa mtaji wake ni takribani trilioni moja.