Zikiwa zimesalia siku chache kuelekea kufunguliwa rasmi kwa maonyesho ya kimataifa ya biashara maarufu kama Sabasaba, Nchi mpya tano zimedhibitisha kushiriki maonyesho hayo yatakayoanza Juni 28 na kumalizika Julai 13.
Meneja Ukuzaji Biashara wa Mamlaka ya Biashara Tanzania (TanTrade) Stephen Koberou amezitaja nchi hizo kuwa ni Marekani, Uingereza, Morocco, Cuba, Uphilipino na Australia na kuongeza kuwa nchi hizo ni mpya kabisa katika maonyesho haya.
Mbali na hayo, Koberou pia amesema katika maonyesho ya mwaka huu, kutakuwepo na siku maalum ya uzinduzi wa Hospitali ya Wafanyabiashara iliyoandaliwa na TanTrade, ambayo amedai ni kitu kipya kabisa kufanyika hapa nchini.
Vilevile, maonyesho ya mwaka huu yatahusisha siku ya sanaa na utamaduni kwa maendeleo ya viwanda, siku ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na siku ya vijana kwa maendeleo ya viwanda.