Umoja wa wakulima wa korosho kutoka mikoa ya Mtwara na Pwani wamedai kilimo cha korosho kipo njiani kufa kama serikali haitatoa asilimia 65 ya ushuru wa mauzo ya korosho nje ya nchi kwa ajili ya maendeleo ya zao hilo kwani kufanya hivyo kunawakandamiza wakulima katika ununuzi wa pembejeo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Tandahimba (Tafa) Faraji Njapuka amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma ambapo ameeleza kuwa, asilimia 35 iliyokuwa ikichukuliwa na serikali ilikuwa sawa kwani wakulima wanakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya manunuzi ya pembejeo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa umoja wa wabanjua korosho wadogo Tanzania Tumpare Magehema amedai kupandishwa kwa tozo hiyo ni mwanzo wa kuua viwanda vidogo ambavyo vilianzishwa na wakulima hivyo wakulima ndio waathirika katika hilo.
Baadhi ya wakulima wa korosho wameomba kukaa pamoja na kuzungumza na serikali ili kufikia makubaliano yatakayonufaisha pande zote mbili na kuinua kilimo hicho.