Home BIASHARA Mambo ya kuzingatia unapoanzisha biashara mtandaoni

Mambo ya kuzingatia unapoanzisha biashara mtandaoni

0 comment 235 views

Kufanya biashara kwenye mtandao ni jambo lenye faida na changamoto zake. Unaweza kuwa na bidhaa nzuri, lakini kila siku, tovuti za kuuza bidhaa kama hizo huanzishwa. Haijalishi kuwa wewe ni muuzaji wa bidhaa wa siku nyingi au wa karibuni, ni wazi kuwa utakutana na changamoto kama wauzaji wengine. Sasa utafanyaje?

Hakuna jibu rahisi, bali ni wazi kuwa makosa unayofanya wakati wa kuendesha biashara kwenye mtandao, ndiyo yanayokugharimu wewe na mapato yako. Kama mfanyabiashara, unatakiwa kufanya yafuatayo ili kufanikiwa.

  1. Kuwahudumia wateja kwa umakini.

Biashara nyingi za mtandaoni zimekufa kutokana na kukosekana kwa umakini kwa watoaji huduma ikiwa ni pamoja na ukosefu wa kitengo cha kuhudumia wateja. Kama ilivyo biashara ya duka ambayo mtu anatakiwa kukaa dukani asubuhi hadi jioni, ndivyo inavyotakiwa kwa biashara ya mtandaoni kwani watu watahitaji msaada, maelezo ya ziada, ushauri na mapendekezo juu ya huduma yako au bidhaa unazouza

  1. Usanifu bora wa tovuti yako ya biashara.

Biashara nyingi za mtandaoni zinakufa kwa sababu ya kukosa umakini wakati wa kusanifisha au kutengeneza tovuti. Tovuti nzuri ni lazima iwe rafiki na rahisi kwa watumiaji wake kwa kuhakikisha inakuwa na muonekano mzuri na rangi isiyoumiza macho, Iwe ina uwezo wa kuonekana vyema katika vifaa vyote kama vile simu, tablet na kompyuta pamoja na kuwa na sehemu ya utafutaji maarufu kama Injini pekuzi. Lakini pia tovuti yako iwe na vipengele vinavyoonyesha mtiririko wa orodha na urambazaji ili kuwarahisishia wateja wako kuchagua aina ya huduma kwa urahisi. Kwa mfano biashara yako inahusika na vifaa vya umeme, majumbani, ofisini, na muziki warahisishie kujua hiki ni kipengele cha vifaa vya muziki na hiki ni masuala ya umeme.

  1. Toa ufafanuzi wa kutosha kuhusu bidhaa ua huduma yako.

Watu wengi wanahitaji kupata maelezo ya kutosha kuhusu bidhaa au huduma unayotoa mtandaoni. Hakuna mtu anayependa kununua kitu ambacho hakifahamu vizuri. Hivyo tambua kuwa kuto itolea vizuri maelezo bidhaa yako kunaweza kusababisha bidhaa yako isinunuliwe kabisa. Kwa mfano Kama ni bidhaa Onyesha picha na eleza kama bidhaa ni mpya au imetumika, gharama yake, ina vitu gani, je, ina udhamini wa muda, imetengenezwa wapi na inapatikana wapi. Haya ni baadhi ya mambo muhimu ambayo endapo utazingatia basi biashara yako ya mtandaoni itaweza kufanikiwa.

  1. Tumia mitandao ya kijamii kujitangaza

Mitandao ya kijamii kama Facebook na Instagram ina umuhimu mkubwa katika kuhakikisha biashara yako ya mtandaoni inafanikiwa. Watu wengi wamekuwa na mwamko mkubwa kuhusu matumizi ya mitandao na hivyo kufanya sehemu hiyo kuwa kama soko. Zipo njia mbili zinazoweza kukusaidia kuitangaza biashara yako kwa njia ya mtandao kama vile:

-Kufungua ukurasa wa biashara yako sambamba na kuitolea maelezo kisha shirikisha kwa watu mbalimbali katika mtandao huo ili waifahamu vizuri.

-Kulipia matangazo ili biashara yako ifahamike sehemu kubwa kwa muda mfupi. Hii ni njia rahisi na ya haraka itakayofanya biashara yako ikue na kufahamika sehemu kubwa ndani ya muda mfupi.

  1. Fahamu wateja na soko.

Biashara yoyote kabla ya kuianzisha hasa za mtandao ni vyema kufanya utafiti kwanza juu ya kile unachotaka kukianzisha. Hakikisha bidhaa unazouza zinaendana na uhalisia wa mazingira na uhitaji wa watu pamoja uwezo wao wa kumudu gharama za manunuzi vinginevyo biashara yako haitoweza kufanikiwa.

  1. Andaa mfumo mzuri wa kulipia na kusafirisha huduma za wateja wako.

Mara nyingi unapouza vitu kupitia mtandao wateja watalipia bidhaa zao moja kwa moja, pia watafahamu jinsi watakavyopata bidhaa husika. Wauzaji wengi hawaweki mfumo rahisi kwa wateja ili waweze kufanya malipo; kwa mfano tovuti za Afrika Mashariki tunategemea kuona njia za malipo kama vile M-Pesa, Airtel Money, Tigopesa, MTN n.k. Pia ni lazima kuwe na mfumo mzuri wa kuwasafirishia au kuwafikishia wateja bidhaa zao. Kwa kufanya hivi utaaminika zaidi na kujiongezea wateja.

  1. Jitangaze ipasavyo.

Kama waswahili wasemavyo biashara ni matangazo, hakikisha unawekeza kiasi cha kutosha kwa ajili ya matangazo.Hii itakusaidia kujipambanisha mbele ya washindani wako wa soko na kujiongezea umaarufu na ukuaji wa biashara yako. Hakikisha unajitangaza katika vyombo vya habari na mabango kwani hii itasaidia biashara yako kufahamika sehemu kubwa zaidi ndani ya muda mfupi.

Ili biashara iweze kukua na kupendwa na watu, ni lazima ionyeshe ushindani dhidi ya watu wengine wenye kufanya biashara kama hiyo. Biashara za mitandaoni zinakabiliwa na ushindani mkubwa hivyo kabla ya kuamua kufanya aina hii ya biashara, ni bora kujipanga vizuri ili kuhakikisha unaweka sokoni bidhaa na huduma bora zaidi.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter