Home AJIRA Wahitimu SUA kupata donge nono

Wahitimu SUA kupata donge nono

0 comment 63 views

Wahitimu wapatao 100 kila mwaka katika chuo cha Kilimo cha Sokoine kilichopo Morogoro wanatarajia kunufaika kupitia gawio la Sh.Bilioni 2 ambazo zitakuwa zikitolewa na Taasisi Binafsi ya Kusaidia Sekta ya Kilimo Nchini (PASS).

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa PASS Nicomed Bohay baada ya kuingia makubaliano na SUA kwa lengo la kuwaandaa kwa vitendo wajasiriamali vijana wanaohitimu katika chuo hicho katika fani mbalimbali hususan kilimo.

Bohay alisema lengo kuu ni kuwawezesha wahitimu hao kupata mitaji pamoja na nyenzo mbalimbali ili kuwajengea hali na uwezo uwezo wa kusimamia miradi ya kilimo na biashara.

Alisema wajasiriamali vijana watakaojihusisha na uzalishaji wa mboga mboga, kwenye mahema, ufugaji wa kisasa wa samaki, kuku, mbuzi, usindikaji na viwanda vidogo vidogo ndio watakaopewa kipaumbele ili kujihakikishia uzalishaji bora wa bidhaa zinazotokana na kilimo kwa ajili ya masoko ya ndani na nje.

“Wenzetu SUA wametoa eneo la kutosheleza kwa miradi ya wajasiriamali vijana kwa lengo la kuhakikisha vijana wetu wanapata mahali pa kuanzia kabla ya kujitegemea”Alisema Bohay.

Kwa upande wake Makamu mkuu wa SUA, Prof, Raphael Chibunda alisema kuwa ushirikiano kati ya PASS na chuo hicho umekuja kwa muda mwafaka na kuwataka wahitimu na watafiti chuoni hapo kuichangamkia fursa hiyo.

“Kwetu sisi mradi huu wa kuwalea wahitimu wetu kwa kuwapatia mitaji, nyenzo na ushauri wa maeneo maalumu ya kutekeleza kile walichokisoma darasani kwa vitendo,ni faraja sana kwani siku zote tumekuwa tukiwaandaa vijana wetu kukabiliana na changamoto za maisha huko mtaani kwa kutumia elimu waliyoipata hapa chuoni”. Alisema Prof. Chibunda

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter