Wakulima mkoani Simiyu wameiomba serikali kushusha chini bei ya mbolea inayozalishwa viwandani ili waweze kuitumia kwani hivi sasa wengi wao wanatumia zile za kienyeji ambazo hazina tija katika kilimo chao. Wakulima hao wamesema hayo katika viwanja vya maonyesho ya nanenane ambayo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi na kuongeza kuwa, kupanda kwa bei ya mbolea za viwandani kumewalazimu wao kutumia mbolea za kienyeji katika kilimo wanachofanya.
Kwa upande wao, baadhi ya wataalam pamoja na wazalishaji wa mbolea za viwandani wamedai japokuwa wanazalisha mbolea kwa wingi, mwitikio wa wakulima kutumia mbolea hizo umekuwa mdogo japokuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa wakulima kutumia mbolea hizo mara kwa mara. Wataalam hao wameshauri wakulima wa hapa nchini kufanya utafiti na kuangalia tofauti ya kutumia mbolea ya viwandani na ile ya kienyeji ili waone tofauti iliyopo.