Takwimu kutoka Benki ya Dunia (WB) zinaonyesha Tanzania inashika nafasi ya 137 kati ya nchi 190 duniani kwa kutokuwa na mazingira rafiki kwa ajili ya biashara huku vikao vya mabaraza ya kibiashara vikielezwa kusuasua. Hayo yameelezwa katika taarifa ya Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira iliyowasilishwa na Mkuu wa wilaya ya Same Rosemary Staki wakati akifungua mafunzo ya mbinu za kusimamia na kuendesha majadiliano kati ya sekta binafsi na ile ya umma yaliyoandaliwa na Chama cha wenye Viwanda, Biashara na Kilimo (TCCIA).
Kufuatia takwimu hizo, Mghwira amewaagiza wajumbe wa mabaraza ya biashara kuhakikisha majukumu yao yanatekelezwa kwa vitendo ili kuchochea zaidi uwekezaji na biashara katika mkoa huo ambao amedai una fursa mbalimbali zikiwemo utalii, viwanda na ardhi ambazo hazijatangazwa vilivyo kwa wawekezaji.
“Ninawaagiza maofisa biashara na wenyeviti wa mabaraza haya kuhakikisha mabaraza ya biashara yanaimarishwa ili yaweze kufanya kazi vizuri pamoja na vyombo vya majadiliano viboreshwe ili kuleta mahusiano mazuri zaidi kati ya sekta ya biashara na sekta ya umma”. Amesema Mghwira.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TCCIA mkoani Kilimanjaro Patrick Shirima amedai moja kati ya sababu kubwa inayopelekea wafanyabishara wafanyabiashara wengi kushindwa kulipa mapato ya serikali ni kukosa umeme wa uhakika, hali ambayo imekuwa changamoto kubwa katika shughuli zao.