Baada ya kushindwa kufikia muafaka kwa muda mrefu, hatimaye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekubaliana kurekebisha sheria ya fedha ili kushusha gharama za miamala inayofanywa na wananchi wanaotembelea nchi nyingine. Wawakilishi kutoka Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda wamefanya mkutano jijini Mombasa, Kenya na kukubaliana kuendeshwa kwa utafiti utakaoruhusu wateja kutoka benki moja kutumia mashine za ATM za benki nyingine kwa gharama nafuu katika nchi jirani.
Gazeti la Business Daily limemnukuu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kumuiya ya Benki za Kenya (KBA) Habil Olaka akisema kuwa mpango huo utainua matumizi ya huduma za fedha kwa wananchi kutoka nchi za jumuiya hiyo nakuongeza kiasi cha malipo kinachofanywa na miamala ya nje ya nchi.
Hivi sasa, gharama ya kutumia ATM iliyo nje ya mipaka ya nchi kwa wateja wa benki ndani ya EAC ni Sh. 5,625 (USD 2,5) lakini mpango huu ukianza kutekelezwa, gharama hizo zinatarajiwa kupungua na kufikia Sh. 1,800 (USD 0.8) kwa kila muamala. Mbali na gharama za kila muamala, benki kuu kutoka kila nchi zitabeba jukumu la kupanga kiwango cha ubadilishaji fedha ili kuepuka hasara zinazotokea pindi mteja anapokuwa nchi jirani.