Benki kuu ya Tanzania (BoT) imeshusha kiwango cha riba kwa mabenki ya biashara kukopa kwenye hazina yake kutoka 9% mpaka 7% ambazo zitaanza kutumika rasmi kuanzia leo mpaka hapo itapofanyiwa mapitio mengine.
Punguzo hilo linatarajiwa kuwanufaisha wafanyabiashara wadogo,wananchi wa kawaida na wafanyakazi wa kada zote ikiwemo wa sekta binafsi ambao watakua na fursa ya kukopa kiasi kikubwa cha fedha kwa muda mrefu wa marejesho. Lakini pia punguzo hilo litakua chachu ya kuinua uchumi kwani wafanyabiashara wengi hasa wenye mitaji midogo watakua na sifa ya kukopesheka.
Ikumbukwe mnamo agosti 23 BoT iliandika barua kwenda kwa mabenki ya biashara iliyoizinishwa na Naibu Gavana anayesimamia sera za uchumi na fedha (EFP) Dk. Yamungu Kayandabila ikizitaarifu benki hizo kuhusu uamuzi huo wa BoT. Pia nakala za barua hiyo zilitumwa kwa mwakilishi mkazi wa shirika la fedha duniani (IMF) pamoja na Kamishina wa mapato wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Kwa mujibu wa barua hiyo, lengo kuu la punguzo hilo ni kukuza kiasi cha mikopo inayotolewa kufanikisha shughuli za uchumi na kwa kuzingatia mwenendo wa mauzo ya hati fungani za serikali lakini pia kuongeza upatikanaji wa fedha kwa wananchi na sekta binafsi ili kufanikisha sera ya uchumi wa viwanda.
Ikumbukwe hii si mara ya kwanza kwa BoT kushusha riba kwa mabenki ya biashara ambapo kwa vipindi tofauti tofauti imeshuka kutoka 16% mpaka 7% inayoanza kutumika leo.