Home KILIMO Waficha karafuu watahadharishwa

Waficha karafuu watahadharishwa

0 comment 129 views

Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Balozi Amina Salim Ali ameahidi kutowafumbia macho wakulima wote walioficha karafuu badala ya kuzipeleka katika Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) kwa ajili ya mauzo kama utaratibu unavyowataka. Balozi Amina Ali ameyasema hayo alipokutana na viongozi pamoja na wananchi katika hafla ya uzinduzi wa uchumaji karafuu msimu wa 2018/19 iliyofanyika visiwani Zanzibar.

Balozi Amina amesema anafahamu wazi kuwa wakulima wengi wamehifadhi karafuu majumbani badala ya kuliuzia shirika hilo huku akidai kuwa, kufanya hivyo ni kurudisha nyuma maendeleo ya taifa kwa kuwa serikali ipo tayari kushirikiana na wakulima na kutatua changamoto zinazowakabili.

“Ni matarajio ya serikali kuwa wote walioweka karafuu nyumbani wataziuza kwa kuwa kuziweka ni makosa ila kwa kuwa tunawajali wakulima wetu tunawasamehe tu”. Amesema Balozi Amina.

Alisema serikali imejipanga kuwapatia wananchi vifaa bora vya kuvunia karafuu yakiwemo majamvi na magunia sambamba na kuhakikisha asilimia 80 ya anayopata mkulima kwa kuuza karafuu kwa ZSTC zinatolewa kama kawaida na kuhakikisha kuwa kunakuwepo na mtiririko mzuri wa ununuzi wa zao hilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba, Hemed Suleiman Abdallah amewataka wananchi kuacha kuuza karafuu kwa njia ya magendo akisisitiza karafuu inayouzwa nje huchangia ujenzi na uendelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo visiwani humo.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter