Wizara ya Kilimo imelitaarifu Bunge kuwa, kufuta tozo 19 kwenye zao la kahawa kumeimarisha bei ya mkulima. Akijibu swali la Mbunge Jasson Rweikiza wa Bukoba vijijini, Naibu Waziri wa Kilimo Omari Mgumba amefafanua kuwa, bei ya kahawa hupangwa kwa kuzingatia masoko mawili ambayo ni soko la bidhaa la New York kwa kahawa aina ya Arabika na soko la London kwa kahawa aina ya Robusta.
“Aidha, kupungua kwa kodi na tozo hizo kumesaidia bei ya kahawa kuwa nzuri ambapo kwa mara ya kwanza katika msimu wa 2017/2018 kahawa ilitoka nchi ya Uganda na kuleta Tanzania kutokana na wakulima wa Uganda kuvutiwa na bei iliyopo Tanzania. Mwenendo wa bei katika masoko hayo una athari za moja kwa moja kwenye soko la kahawa na bei anayopata mkulima”. Ameeleza Naibu Waziri Mgumba.
Katika maelezo yake, Naibu huyo pia amesema bei ya kahawa aina ya Arabika imeshuka kutoka Sh. 4,000 kwa kilo mwaka 2016/2017 na kufikia Sh. 3,800 kwa kilo mwaka 2017/2018. Mgumba ametaja mojawapo ya sababu ya kushuka kwa bei kuwa ni wanunuzi pamoja na viongozi wa ushirika kutoelewa maelekezo yaliyotolewa na serikali kuhusu kuuza bidhaa hiyo moja kwa moja sokoni.