Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIBIASHARA M-Pesa na Mastercard kurahisisha manunuzi mtandaoni

M-Pesa na Mastercard kurahisisha manunuzi mtandaoni

0 comment 100 views

Kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania pamoja na Mastercard kwa ushirikiano na Benki ya BancABC wameungana na kuzindua kadi mpya ya mastercard iitwayo Virtual Card itakayowawezesha watumiaji wa huduma za M-Pesa kufanya manunuzi ya mtandaoni kwa urahisi kupitia kadi hiyo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika katika ukumbi wa Ramada Encore Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Plc, Hashim Hendi amesema kuwa wameamua kurahisisha huduma kwa watumiaji wa huduma ya M-Pesa wapatao Milioni 8.2 wakihudumiwa na mawakala wapatao laki moja waliosambaa nchi nzima, ikiwa ni katika kuleta mapinduzi ya manunuzi ya mtandaoni pamoja na kuwahakikishia watumiaji wa huduma ya M-Pesa usalama wa fedha zao.

“Huduma ya M-Pesa kutoka Vodacom ina wateja zaidi ya milioni 8.2 huku ikiwa na zaidi ya wakala laki moja waliotapakaa nchi nzima, hii inawezesha upatikananaji wa uhakika wa huduma za kifedha, lakini imekuwa ni ngumu pale linapokuja suala la kulipia manunuzi mtandaoni haswa kupitia tovuti za kimataifa. Uzinduzi na ufanyaji kazi wa Virtual Card kupitia M-Pesa utaleta mapinduzi katika kuwezesha watanzania kufanya manunuzi mtandaoni pamoja na kuwahakikishia usalama wa taarifa zao za kibenki” Alisema Hendi.

Uunganishwaji wa intaneti katika bara la Afrika unatajwa kuwa chanzo cha upatikanaji mkubwa wa simu janja (Smartphone), ambapo ukuaji huo umekuwa ukienda sambamba na ongezeko la huduma za kimtandao ikiwa ni pamoja na manunuzi, matumizi ya mitandao ya kijamii, maudhui ya kidijitali na M-Commerce.

Akielezea namna Virtual Card itakavyotumika kufanya manunuzi ya mtandaoni, Hendi amesema kuwa kadi hiyo itawawezesha wateja wa M-Pesa kufanya malipo ya aina mbalimbali kupitia tovuti za nje na za ndani ya nchi, ama kufanya malipo kwa App zinazohitaji matumizi ya Mastercard bila ya uhitaji wa akaunti ya benki au kadi ya Mkopo (Credit Card), huku huduma hiyo ikitarajiwa kuwepo kwenye menu ya M-Pesa pamoja na App ya M-Pesa na kuongeza kuwa mteja ataweza kutumia kadi hiyo mara baada ya kuwa imeshajazwa pesa.

Kwa upande wake Rais wa Mastercard kwa divisheni ya Ukanda wa Sahara Bw. Raghav Prasad amesema kuwa uwepo wa huduma za kifedha kwa njia ya mtandao umesaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha utoaji huduma kwa kuwa watu wengi wameweza kununua bidhaa au kupata huduma pasipo kuwa na fedha mkononi ambayo ni huduma jumuishi na kuongeza kuwa miaka ya mbeleni kila huduma itaweza kutolewa kwa kutumia simu ya mkononi kwa sababu hiyo ndio mtu anakuwa nayo kila mahali aendako.

Tanzania imekuwa ikipiga hatua kubwa katika kukuza huduma za mtandaoni pamoja na kuwahakikishia usalama watumiaji wake ambapo takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 15.8 ya watanzania mwaka 2009 walikuwa wanashikilia uchumi wa nchi idadi ambayo imepanda hadi asilimia 65.3 kwa mwaka 2017 ikiwa imechangiwa na uwepo wa huduma za kifedha kwa simu za mkononi ikiwemo ya M-Pesa.

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter