Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI Mavunde ahimiza vijana kuchangamka

Mavunde ahimiza vijana kuchangamka

0 comment 107 views

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu) Anthony Mavunde ametoa wito kwa vijana wilayani Kahama kuchangamkia fursa ya mradi wa kitalu (maarufu kama Greenhouse) na kuinua uchumi wao kupitia kilimo cha matunda na mbogamboga ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupatiwa mikopo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Naibu Waziri Mavunde amesema hayo katika ziara yake wilayani Kahama mkoani Shinyanga wakati akizungumza na wananchi wa kata za  Mpunze na Mwendakulima na kuongeza kuwa, kupitia mradi huo unaotekelezwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu vijana wengi watapata nafasi ya kujiendeleza na kuinua uchumi wao kupitia kilimo cha mbogamboga na matunda.

Mavunde amedai kuna takribani mifuko 19 ya uwezeshaji wananchi inayotoa mikopo na TADB ipo tayari kutoa huduma kwa kundi la wakulima wadogo. Naibu huyo pia ameahidi kupeleka maofisa wa benki hiyo ili kuhakikisha vijana wanapatiwa mikopo yenye gharama nafuu itakayowawezesha kufanya kilimo kwa tija zaidi.

Pamoja na hayo, Mavunde amemtaka Mkurugenzi wa halmashauri ya Kahama kugawa eneo lililotengwa na halmashauri hiyo kwa wakazi walio kwenye vikundi ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao za kilimo na kutaja mdau mkubwa wa soko la mazao yao ni mgodi wa Buzwagi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter