Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ya Hai, Elia Machange amesema serikali kupitia Mfuko wa Umwagiliaji wa Wilaya (DIDF) imetoa Sh. 383 milioni kwa Halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika mradi wa umwagiliaji wa zao la mpunga skimu ya Kikavu chini. Machange amedai kuwa maboresho katika mradi huo yanalenga kuwashawishi wananchi wengi zaidi kufanya kilimo.
“Kabla ya kukarabatiwa mradi huu, eneo hili lilikuwa na uwezo wa kumwagiliwa hekta 441 na baada ya ukarabati eneo linalomwagiliwa kwa sasa ni hekta 541. Kwa ujumla mazao yanayolimwa hapa ni pamoja na mahindi, maharage, mpunga, mbogamboga pamoja na ndizi”. Ameeleza Machange.
Kaimu huyo ameongeza kuwa hadi sasa, mradi huo unawanufaisha wakulima wapatao 2,100, kati yao 500 wakiwa wanawake, wanaume 450 pamoja na vijana 1,150 ambao wameweza kujiajiri kupitia kilimo cha umwagiliaji Machange pia ameeleza kuwa fedha za kuboresha skimu hiyo iliyoanzishwa rasmi mwaka 2017 ikiwa na hekta 641 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji zimetolewa na DIDF.