Waziri wa Kilimo Dk. Charles Tizeba amesema kuwepo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kiasi kikubwa kumewasaidia wakulima wadogo na wale wa kati na kuwawezesha kupata bei nzuri ikilinganishwa na bei zilizokuwa zinatolewa na wafanyabiashara wanaponunua mazao yao yakiwa shambani kwa kutumia vipimo visivyo sahihi. Dk. Tizeba amesema hayo wakati akifungua mkutano mkuu wa wadau wa korosho ambapo ameeleza kuwa uwepo wa vyama vingi vya ushirika hivi sasa ni matokeo ya elimu inayotolewa kuhusu umuhimu wa ushirika.
“Ni wazi kuwa katika kipindi cha miaka miwili hivi, imani kwa vyama vya ushirika imeongezeka na vyama vingi vimeendelea kuundwa hasa vile vya kuweka na kukopa (Saccos)”. Amesema Waziri huyo.
Katika mkutano huo, Waziri Tizeba pia ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika zao la korosho ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa usimamizi wa zao hilo, utaratibu mzuri wa ununuzi na usambazaji wa pembejeo za ruzuku, usimamizi wa karibu unaofanywa na viongozi wa ngazi mbalimbali serikalini pamoja na nia ya wakulima kujikita katika kilimo cha korosho katika maeneo mapya na asilia.
Waziri Tizeba amesisitiza kuwa kiwango cha uzalishaji kikiendelea kama ilivyo hivi sasa, kuna uwezekano wa kuzalisha zaidi ya kiwango cha sasa na kuwa na malighafi itakayotumika kwa mwaka mzima kwa kuuza kwa viwanda vya ndani na nje ya nchi.