Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amesema ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa upanuzi wa bandari, ujenzi wa magati na kuongeza kina cha kupakia na kupakua mizigo kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Naibu huyo amesema hayo baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo na kuona kuwa, kiwango cha asilimia 42 ya mradi huo tayari kimefikiwa.
Katika maelezo yake, Mhandisi Nditiye amebainisha kuwa ilibidi kufanya maboresho katika mradi huo ili kuendana na matakwa ya mradi kuweza kubeba mizigo mizito na inatarajiwa kuwa, ujenzi huo utakamilika mwezi Juni mwakani. Mbali na muda wa mkataba wa mradi huo, ujenzi wa gati namba moja ulikuwa unaendelea na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Karim Mataka amedai maendeleo ya mradi ni mazuri japokuwa kumekuwa na changamoto ya udongo laini baharini kwenye eneo la ujenzi wa mradi huo, hali ambayo imewalazimu kuimarisha eneo hilo ili bandari iwe na uwezo wa kubeba mzigo wa kontena mpaka tano zilizopandana kutokea chini kwenye eneo la kupakia na kupakua mizigo.