Home VIWANDAUZALISHAJI Mradi wa EADD kukuza soko la tasnia ya maziwa nchini

Mradi wa EADD kukuza soko la tasnia ya maziwa nchini

0 comment 115 views

Na Ismail Ngayonga-MAELEZO-DAR ES SALAAM

TAKWIMU ya zao la maziwa nchini zinaonyesha kuwa, Tanzania inazalisha maziwa lita bilioni 2.4 kwa mwaka, ambapo 70% huzalishwa na Ng,ombe wa asili ambao uzalishaji wake ni kati ya lita moja mpaka lita tano kwa siku.

Wakati Shirika la Afya Duniani  (WHO) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) likipendekeza kiwango cha unywaji maziwa kwa Binadamu ni  lita 200 kwa mwaka, imebainika katika Tanzania unywaji wa maziwa  kwa mwaka ni asilimia 47, hii na sawa na chini ya robo ya kiwango kinachopendekezwa.

Taarifa hizo za WHO na FAO zinaongeza kuwa Kenya inaongoza Afrika kwa uzalishaji wa maziwa ya ng’ombe wakati Tanzania ikishika nafasi ya tisa, ambapo Kiwango cha unywaji wa maziwa kwa Tanzania kwa kila mtu ni chini ya lita 50 kwa mwaka wakati Kenya ikifikia lita 130.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 zinazokabiliwa na changamoto ya kuwa na watoto wenye udumavu, ugonjwa ambao unachangiwa kwa kiwango kikubwa na lishe duni wanazozipata watoto walio chini ya miaka mitano.

Sababu kubwa inayofanya watoto hao kudumaa ni ukosefu wa vyakula vyenye virutubisho mwilini, ikiwemo maziwa ambayo yana virutubisho vyote muhimu kwa ujenzi wa afya ya binadamu ikiwemo protini, mafuta, madini, vitamin na sukari ya asili ya lactose na maji.

Inaelezwa kuwa maziwa yanayoingia viwandani kusindikwa ni asilimia 3 pekee ndiyo inayozalishwa huku kukiwa na viwanda 76 vyenye uwezo wa kusindika  lita 640,000 kwa  siku, lakini kwa sasa viwanda vinavyosindika Maziwa ni  63 tu vyenye uwezo wa kusindika lita 170,000 za Maziwa kwa siku.

Ili kubaliana na changamoto hiyo, Serikali imeendela kupitia sheria za sekta ya mifugo ili ziendane na Sera ya Ugatuaji wa Madaraka na kuboresha mazingira na huduma za biashara ya mifugo na mazao yake.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Hotuba ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina anasema Serikali kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Sekta ya Maziwa Afrika Mashariki na Kati-EADD II) kwa kushirikiana na taasisi ya Heifer International umetoa mafunzo kwa wafugaji 25,659 kuhusu ufugaji bora wa ng‟ombe wa maziwa katika nyanja za uzalishaji mifugo, ulishaji, tiba na afya ya mifugo.

Anaongeza kuwa Mradi huu umeunda jumla ya Vyama vya Ushirika vya Msingi 37 na kuunda vitovu vya biashara ya maziwa ambapo vimeweza kuwa na mapato ya takriban shilingi bilioni 2 kwa mwaka.

“Wafugaji hao walitoka katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe na Songwe ambapo umewawezesha wafugaji kuanzisha vituo 11 vya kisasa vya kukusanya maziwa vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.4 na fedha hizi zilizotolewa kama ruzuku kwa wafugaji zitagharamia ununuzi wa matenki 11 ya maziwa, jenereta 11, vyombo na vifaa vya kusafirishia maziwa na ujenzi wa vituo” anasema Mpina.

Aidha Waziri Mpina amesema ili kupanua wigo wa masoko ya maziwa ya wafugaji, EADD inashiriki katika kukiboresha Kiwanda cha Wafugaji Njombe kuwa cha kisasa na kukipanua kutoka uwezo wa kusindika lita 6,000 hadi 20,000 kwa siku.

Waziri Mpina anasema katika mwaka 2017/2018, mradi wa EADD II umeanzisha program ya unywaji maziwa shuleni kwa lengo la kuwafikia wanafunzi wa shule za awali na msingi 10,000 ambao watakunywa maziwa mls 200 kwa kila mtoto kwa siku za shule.

Anaongeza kuwa kupitia Programu hiyo, hadi kufikia kufikia Machi 2018, wanafunzi wapatao 11,398 wamenufaika na mradi huu kwa siku 4 kati ya siku 5 za shule katika shule 17 za wilaya za Rungwe, Njombe, Wanging‟ombe, ambapo kupitia mradi huo masoko ya maziwa ghafi yameongezeka kwa kiwanda cha Njombe kutoka lita 3,200 hadi kufikia lita 5,600 kwa siku.

Akifafanua zaidi Waziri Mpina anasema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa Sekta Binafsi ili kuwasaidia wafugaji kupanua wigo wa masoko ya maziwa na ujenzi wa viwanda vya maziwa sambamba na kuwasaidia katika katika kuanzisha vituo vya kisasa vya kukusanya maziwa ili wafugaji wengi zaidi waweze kuvifikia kwa karibu zaidi.

Ili tasnia ya maziwa nchini iweze kupiga hatua ni wajibu wa Serikali kupitia Bodi ya Maziwa kuhamasisha sekta binafsi kwa lengo la kuimarisha uzalishaji, ukusanyaji na usindikaji wa maziwa sambamba na utoaji wa elimu kuhusu ufugaji wa kisasa kwa wafugaji wadogo nchini.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter