Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Savings Bank Foundation for International Cooperation (SBFIC) nchini, Steven Noel Safe amesema shirika hilo lipo kwenye mikakati ya kutoa elimu ya fedha kwa taasisi ndogo za kifedha nchini ili kutafuta ufumbuzi bora wa masuala ya kuweka na kukopa fedha. Safe amesema hayo kwenye hafla ya ufunguzi wa ofisi za shirika hilo na kusema wanalenga kutoa elimu kwa wananchi hususani wajasiriamali kuhusu namna ya kuweka na kukopa kwenye taasisi za fedha.
Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa mkakati huo utakaoanza mwakani unawalenga walimu wa masuala ya elimu ya fedha hasa walioko mashuleni kwa ajili ya wanafunzi, maofisa ushirika kwa ajili ya vyama vya kuweka na kukopa fedha pamoja na maofisa maendeleo ya jamii watakaoelimisha vikundi vya kijamii vinavyokopa kwenye halmashauri.
“Changamoto kubwa ni watanzania tunapopata miradi tusifikirie itadumu milele, tunatakiwa tuifanye kwa weledi ili tuendelee. Pia tumezoea wageni wanaotoa posho na hatutaki kuchangia chochote na wakiondoka miradi mingi inakufa na hakuna maendeleo yoyote. Kwa elimu tunayotoa, tunataka mwananchi ajue kila kitu ili achague mwenyewe akakope wapi kwa riba nafuu”. Ameeleza Safe.
Akielezea mikakati ya kimenejimenti ya kukuza biashara ya taasisi husika, Safe amesema hadi sasa, shirika hilo limefanya kazi na Benki ya Posta (TPB), Karagwe Development and Conservation Agency (KARUDECA), Tanzania Association of Micro Finance Institutions (TAMFI), SELF Microfinance Fund na Tume ya Ushirika Tanzania.