Home BIASHARA Watakaoingiza mafuta kimagendo kuchukuliwa hatua

Watakaoingiza mafuta kimagendo kuchukuliwa hatua

0 comment 107 views

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezitaka kamati zinazoshughulika na ulinzi na usalama katika ngazi za mikoa na wilaya kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika wanaingiza bidhaa za chakula na mafuta ya kupikia hapa nchini kwa njia za magendo. Waziri Majaliwa ameagiza mamlaka husika kuendelea kudhibiti uingizwaji holela wa bidhaa mbalimbali za vyakula visivyo na virutubisho yakiwemo mafuta ya kupikia, huku wakihakikisha kuwa adhabu kali zinatolewa na kwa wafanyabiashara walio na mazoea ya kuingiza bidhaa hizo nchini.

Majaliwa ametoa maagizo hayo bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge Zainab Vullu aliyehoji kama uagizwaji wa mafuta ya kupikia kutoka nje unazingatia Sheria iliyopitishwa na serikali ambayo inayolazimisha vyakula na mafuta ya kula kuwekwa virutubisho.

Katika majibu yake, Waziri Mkuu amesema ipo Sheria (Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219) inayohusu udhibiti wa vyakula yakiwemo mafuta ya kupikia ambayo ipo chini ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na imeweka utaratibu wa kudhibiti uzalishaji, uagizaji, usambazaji pamoja na uhifadhi wa mafuta.

“Sheria hiyo pia inataka vyakula vyote vikiwemo vile vilivyoagizwa kutoka nje ya nchi na vinavyozalishwa hapa nchini yakiwemo mafuta ya kupikia, lazima viwekewe virutubisho. Wafanyabiashara wanapaswa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa ili kulinda afya ya mlaji”. Amesema Waziri Majaliwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter