Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) haitavumilia vitendo vya wanafunzi kupata mkopo kwa njia za udanganyifu na kusababisha wengine walio na vigezo kukosa fursa hiyo. Waziri Ndalichako amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe Juma mjini Unguja.
“Na wengine ambao wanachukua mkopo hata kimsingi ni ile ubinafsi lakini hawakuwa na uhitaji hizo fedha wangewaachia watoto ambao hawana uwezo kiukweli kweli, kuna watu wengine mpaka wanadanganya wengine walikuwa wanajipa hata uyatima mpaka siku hizi inabidi tuwe tunafuatilia vyeti mtu akisema yatima tujiridhishe. Lakini watu walikuwa wanafika mahali wanadanganya ili wapate mikopo kwa hiyo mimi niombe tu tuwe na uzalendo, tuangalie mikopo tumeweka kwa walio na uhitaji kwa hiyo wewe kama huna uhitaji sio lazima wala huna sababu ya kwenda kuchukua tuachie watoto ambao bila huo mkopo hawawezi kusoma kabisa.” Ameeleza Ndalichako.