Mataruma milioni 1.2 ambayo yatatumika katika ujenzi wa reli ya kisasa maarufu kama SGR kwa kipande cha Dar es Salaam–Makutupora yatazalishwa hapa nchini katika kiwanda kilichopo Soga mkoani Pwani ambapo mataruma hayo hutengenezwa kwa kutumia kokoto, mchanga, maji pamoja na saruji. Akizungumza wakati wa kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa reli hiyo, Meneja Mradi (Dar es salaam–Morogoro) Machibya Masanja, amesema kuwa, kwa siku moja, kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha mataruma 1,080 na hadi kufikia sasa kimezalisha mataruma yasiyopungua 27,000.
“Watu wamekuwa wakisema tunaagiza mataruma kutoka nje, hapana tunayazalisha hapa hapa kwa kutumia malighafi za viwanda vya ndani na kila taruma lina uzito wa kilo 380”. Ameeleza Masanja.
Masanja amefafanua kuwa kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro, wanatarajia kuzalisha mataruma 500,100 huku kipande cha Morogoro–Makutupora wakizalisha mataruma takribani 703,300.