Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Joseph Kakunda amesema takribani Sh. 40 bilioni kati ya Sh. 528 bilioni zinazotarajia kununua tani 160,000 za korosho zilizopo katika maghala zimetumika kununua korosho kwa wakulima 40,000. Waziri Kakunda amesema hayo jijini Dar es salaam alipotembelea maonyesho ya bidhaa za viwandani ambayo yatafunguliwa rasmi leo katika viwanja vya Sabasaba.
Katika maelezo yake, Waziri Kakunda amesema takribani tani 275,000 za korosho zinatarajiwa kuvunwa msimu huu ambapo hadi sasa, wakulima tayari wamevuna na kuuza tani 160,000 huku tani nyingine 100,000 zikitarajiwa kuvunwa mwezi huu.
“Zoezi la kuwalipa wakulima linakwenda vizuri mpaka jana zaidi ya Sh. 40 bilioni zilikuwa zimetumika. Changamoto tunayokabiliana nayo ni upungufu wa mashine za kubangulia korosho, kwa hiyo tumepanga kuhifadhi korosho wakati tukisubiri maelekezo mengine ya viongozi wetu”. Amesema Waziri huyo.
Aidha, Waziri huyo amesema wanaendelea kupambana na wafanyabiashara wanaodhulumu wakulima kwa kununua mazao yaliyopo shambani na kuweka wazi kuwa hadi sasa, watu 20 wamefikishwa mahakamani kwa kosa hilo.
“Wale waliopanga kuwadhulumu wakulima tunawashughulikia. Kila mkulima anayeleta korosho zake tunakwenda kuangalia shamba lake, tumewadhibiti wale wanaoleta korosho wanazowadhulumu wakulima”. Amesisitiza Waziri Kakunda.