Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Innocent Bashungwa amesema wizara hiyo imeweka mkakati wa kuinua kilimo cha chai kwa kuanzisha soko la uhakika. Bashungwa amesema hayo wilayani Mufindi mkoani Iringa ambapo alitembelea wakulima wadogo na wakubwa wa chai.
“Ni wakati sasa wa kuona zao la chai linamnufaisha mkulima. Nimeshawaelekeza Bodi ya Chai Tanzania haraka iwezekanavyo kuleta ule mkakati wa kitaifa wa kufufua zao la chai nchini na tutoke kwenye uzalishaji wa tani 34,000 za sasa na angalau kufikia tani 40,000 ili tuweze kuwafikia wenzetu wa Kenta”. Amesema Naibu Waziri huyo na kuongeza kuwa:
“Uzalishaji wa chai kwenye upande wa masoko tayari tumeshaagiza Bodi ya Chai kufikia Mei mwaka huu mkakati wa kuanzisha soko la chai jijini Dar es salaam unakamilika na kuhakikisha chai inauzwa nchini ili mwaka wa fedha wa 2019/2020 unapoanza Julai tunakuwa na mnada ili gharama za usafirishaji chai nje zinapungua, na faida ile ije kumsaidia mkulima”. Ameeleza Bashungwa.
Kwa upande wake, Mjumbe kutoka Bodi ya Chai, Dk. Emmanuel Simbua amesema kwa mwaka huu, mchakato wa upangaji bei unafanyika kwa kuwashirikisha wadau wote. Mjumbe huyo pia ameahidi kuwa, viwango vya bei elekezi ya ununuzi wa chai kutoka kwa wakulima vitabadilishwa.