Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema serikali italipa deni la Sh. 241 milioni ambalo Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) inadaiwa na Mamlaka ya Ndege ya Zanzibar. Mhandisi Nditiye ametoa ahadi hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge Jaku Hashim Ayoub aliyehoji ni lini serikali italipa deni hilo linalodaiwa tangu mwaka 2007.
“Ni kweli tunakumbuka na kutambua deni la ada ya utuaji ambayo ATCL inadaiwa, deni hilo litalipwa baada ya mamlaka ya ukaguzi ikikamilisha uhakiki, ATCL ilikuwa na madeni mengi ambayo imekuwa ikiendelea kulipa baada ya kufanyiwa uhakiki”. Amesema Naibu Waziri huyo.
Hata hivyo, kabla ya kuuliza swali lake la msingi, Mbunge Ayoub alitoa pongezi kwa serikali kwa kufuta VAT kwenye umeme Zanzibar.
Akijibu maswali ya nyongeza, Naibu Nditiye amesisitiza kuwa, lengo kubwa la serikali kupitia ATCL ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya usafiri wa anga kwenye kituo chochote kilicho na maslahi ya biashara.
“Hata hivyo ATCL inatumia kituo cha Dar es salaam kama kitovu ili kuwa na muungano wa kupeleka abiria sehemu nyingi na kukidhi mizania ya kibiashara”. Amesema Mhandisi Nditiye.