Home VIWANDAMIUNDOMBINU Ujenzi SGR wamfurahisha Dk. Kijaji

Ujenzi SGR wamfurahisha Dk. Kijaji

0 comment 100 views

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji amesema serikali imedhamiria kukamilisha mradi mkubwa wa reli kwa kiwango cha kimataifa (SGR), ambao hadi sasa, umegharimu zaidi ya Sh. 2 trilioni. Dk. Kijaji amesema hayo baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa reli hiyo kutoka jijini Dar es Salaam hadi Soga, Morogoro ambapo ameshuhudia maendeleo makubwa.

Akiwa katika eneo hilo, Dk. Kijaji ameeleza kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi na kutoa pongezi kwa mkandarasi, kampuni ya Yapi Merkezi, kwa kutekeleza ujenzi huo kwa viwango vya hali ya juu. Naibu Waziri huyo ameelezwa kuwa, treni ya kwanza kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro inatarajia kufanyika Novemba mwaka huu ikiwa kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa.

“Ninampongeza sana Mhe. Rais Dt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake kubwa na kuamua kwa dhati kutekeleza mradi huu mkubwa na miradi mingine, ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji ya Mto Rufiji, ambayo kukamilika kwake kutachochea uchumi wa viwanda. Tunakwenda kwenye Tanzania ya viwanda, tutakuwa na viwanda kila mahali, tumeanza ujenzi wa mradi wa umeme wa megawati 2,115, viwanda vitazalisha bidhaa ambazo zitahitaji miundombinu ya usafirishaji, reli hii itatumika na tunatarajia ifikapo mwaka 2025, Tanzania itakuwa ni nchi yenye kipato cha kati”. Amesema Dk. Kijaji.

Naye Meneja wa mradi huo kipande cha Dar es salaam-Morogoro, Mhandisi Machibya Masanja amesema ujenzi wa reli hiyo umekamilika kwa asilimia 42 na kuongeza:

“Mradi wetu unaenda vizuri na kwa wakati, zoezi la ujenzi na utandikaji reli tumeanza katika jiji la Dar es salaam na unaendelea vizuri ambapo ujenzi wa daraja hilo umekamilika kwa asilimia 55 na utandikaji wa reli katika jiji hili utafikia kilometa 10 mwishoni mwa mwezi Februari”. Ameeleza Mhandisi Masanja.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter