Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba amesema Wizara hiyo imetenga zaidi ya Sh. 10 bilioni kwa ajili ya kuendeleza zao la michikichi mkoani Kigoma na vilevile mikoa mingine yenye uwezo wa kuzalisha zao hilo katika mwaka ujao wa fedha. Mgumba amesema hayo ziarani Kigoma na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akifafanua namna ambazo Wizara hiyo imejipanga kuimarisha zao hilo.
“Mhe Waziri Mkuu tusingeweza kusubiri hadi mwezi wa saba kwa ajili ya kupitisha bajeti badala yake tayari tumetumia mbinu zingine kwa kutumia fedha za matumizi ya kawaida (OC) kwa ajili ya kuanza kutekeleza azma ya serikali ya kuendeleza zao la michikichi na kumaliza tatizo la mafuta”. Amesema Naibu Waziri huyo.
Pamoja na hayo,Mgumba ameelekeza pongezi kwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga taifa, pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Magereza kwa ushirikiano ambao wametoa katika jitihada za kuendeleza zao la michikichi.
“Kama unavyofahamu mchakato wa kuandaa miche ya michikichi unachukua zaidi ya mwaka mmoja na nusu kuanzia kuchavisha mpaka kuwa mche kwa ajili ya kupeleka kwa wakulima, hivyo ushirikiano huo tunaoupata ni utimilifu wa uratibu wa zoezi hili”. Amesema Naibu Waziri Mgumba.