Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amewaeleza wabunge wakati akiwasilisha bajeti ya mwaka 2019/20 kuwa, serikali imetenga Shilingi Milioni 500 na kupokea Shilingi Bilioni 50 kutoka nje ya nchi ili kutatua changamoto ya foleni jijini Dar es salaam.
Dk. Mpango ameeleza kuwa fedha hizo zitatumika kujenga barabara za juu (flyovers) za Chang’ombe, Uhasibu, Kamata, Morocco, Mwenge, Magomeni, Tabata na Buguruni. Pia ametaja barabara nyingine kuwa ni makutano ya Kinondoni/Ally Hassan Mwinyi na Kenyatta na Salendar (Ally Hassan Mwinyi/Un Road Jet).
Waziri huyo amechambua bajeti hiyo kwa kueleza kuwa, Shilingi Bilioni 4 zimetengwa kwaajili ya kufanya upembuzi wa awali wa ujenzi wa reli ya mjini (DSM Commuter Trains), huku Shilingi bilioni mbili zikiwa zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa mabasi yaendayo kasi (Dart), ambao kwa awamu ya kwanza wilayani Kinondoni, umekumbwa na changamoto mbalimbali. Kuhusu usafiri wa maji, Waziri Mpango amesema serikali inatarajia kumalizia malipo ya kivuko kipya cha Magogoni-Kigamboni na kulipa deni la ukarabati wa MV Kigamboni.