Meneja Uendelezaji Biashara wa Benki ya NMB makao makuu, Masato Wasira ameeleza wakati wa mkutano wa wadau wa maji uliofanyika Dodoma kuwa, hadi sasa benki hiyo imeunganisha taasisi zaidi ya 300 na halmashauri 180 zilizopo nchini katika mfumo wa ulipaji na ukusanyaji mapato serikalini (GePG).
Wasira amesema wateja wanaweza kufanya malipo kwa njia ya simu, kwa mawakala wa NMB zaidi ya 6,000 au katika matawi 220 ya benki hiyo kupitia mfumo huo wa GePG ambapo hadi sasa mamlaka za maji 22, idara tano za maji, na bodi za mabonde ya maji 7 zipo katika mfumo huo.
Pamoja na hayo, pia amesema kuwa NMB imetajwa na taasisi ya kimataifa inayojulikana kama Euromoney kwa mara ya sita kuwa ni benki bora kutokana na kutoa huduma bora kwa wafanyabiashara, wakulima, makampuni, taasisi na vilevile serikali. Kwa mujibu wa Meneja huyo, benki ya NMB ina wateja zaidi ya milioni mbili na nusu na inapatikana katika wilaya zote nchini. Benki hiyo imeajiri wafanyakazi zaidi ya elfu tatu.