Mwenyekiti wa Saccos ya Wanawake Wajasiriamali Tanzania (TASWE-Saccos), Ane Matinde amesema mojawapo ya changamoto inayowakabili wajasiriamali hasa wanawake katika kukuza biashara zao ni viwango vikubwa vya riba kwenye benki zinazotoa mikopo. Matinde amesema kuwa kuelekea uchumi wa viwanda, serikali inatakiwa kuangalia suala hilo ili kunusuru sekta za biashara na viwanda.
TASWE-Saccos ni taasisi ya kifedha inayojitegemea ambayo inajihusisha na kuweka akiba pamoja na kutoa mikopo. Taasisi hiyo inawawezesha wanachama kununua hisa, kuwa na akaunti za kuweka fedha ambazo baadae huwasaidia kupata mikopo kwa bei nafuu na vilevile kushiriki katika fursa za uwekezaji na kuendeleza uhuru wa kifedha.
Taasisi hiyo imewanufaisha wajasiriamali takribani 289 na kusaidia asilimia 62 kati ya hao kukuza biashara zao na wengine wakipata masoko katika nchi ya Comoro. Pamoja na hayo, taasisi hiyo pia imetoa mafunzo kwa wajasiliamali zaidi ya 300 katika matawi yake 13 hapa nchini. TASWE imefanya maonyesho yake ya pili ya kimataifa na kuwaleta pamoja washiriki kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Comoro na Tanzania.