Home VIWANDANISHATI Serikali kuwajengea uwezo wananchi katika masuala ya mafuta, gesi

Serikali kuwajengea uwezo wananchi katika masuala ya mafuta, gesi

0 comment 99 views

Na Immaculate Makilika- MAELEZO

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea na mkakati wake wa kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kupata taaluma na kuweza kushiriki kwenye sekta ya mafuta na gesi.

Akizungumza Bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuvitumia vyuo vilivyopo nchini kuwajengea uwezo wa kitaaluma wananchi katika masuala ya utafutaji, uendelezaji, uchakataji, usafirishaji na usambazaji wa mafuta na gesi asilia.

Naibu Waziri Mgallu alisema, “Kwa mfano mwaka 2010 Kampuni ya Petrobras ilitumia dola za kimarekani 350,000 sawa na shilingi milioni 780 kufundisha na kukipatia Chuo cha VETA Mtwara vifaa vya mafunzo. Aidha, kupitia mpango huo, wanafunzi 50 na wakufunzi 2 walifundishwa kwenye fani ya umeme na makanika”.

Aidha, Kampuni ya Statoil imekuwa ikifadhili mafunzo mbalimbali kwa ngazi ya vyuo, ambapo mwaka 2013 ilifadhili wananchi 9 kusoma Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika masuala ya fedha na uchumi wa mafuta ya gesi asilia.

Sambamba na hilo, mwaka 2012 Kampuni ya BG iliendesha mafunzo mbalimbali katika Chuo cha VETA mkoani Mtwara, ikiwa ni pamoja na ufadhili wa mwaka 2012/2013 uliotolewa na iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini  kwa wanafunzi 50 katika chuo hicho.

Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) imefungua klabu 32 za mafuta na gesi katika shule za sekondari za mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo la kutoa elimu inayohusu tasnia ya mafuta na gesi asilia pamoja na namna inavyoweza kuwanufaisha kupitia fursa zinazotengenezwa na tasnia hiyo katika maeneo yao.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter