Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Samuel Gwamaka ametoa wito kwa wadau wote kutekeleza agizo la kuacha matumizi ya mifuko ya plastiki lililotolewa na serikali huku akisisitiza kuwa Baraza hilo limedhamiria kufuatilia zuio hilo kwa kusimamia Sheria za Mazingira pamoja na Kanuni zake.
“Tutasimamia Sheria kwa nguvu zetu zote bila ubaguzi. Tutatumia Sheria bila kujali nafasi ya mtu katika jamii, cheo, rangi au mahali anapotoka”. Ameeleza Mkurugenzi huyo.
Dk. Gwamaka amesema kutokana na uwepo wa ofisi za Baraza hilo kila sehemu hapa nchini, usimamizi wa zuio hilo utaanza katika ngazi ya kata hadi kitaifa, hivyo kuwataka wadau kuzingatia zuio hilo ili kuepukana na usumbufu wowote.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu Msaidizi wa kiwanda cha kutengeneza karatasi kilichopo Mufindi, Gregory Chongo amesema kiwanda chao kina malighafi za kutosha kutengeneza mifuko mbadala hivyo kuwasisitiza wadau kutekeleza agizo walilopewa na serikali itakapofika tarehe 1 Juni.
Siku chache zilizopita akiwa bungeni Dodoma, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alitangaza serikali kupiga marufuku utengenezaji, uingizaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kwa shughuli mbalimbali kuanzia Juni mosi mwaka huu.