Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amekagua na kutoa elimu ya vitambulisho kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo katika maeneo mbalimbali wilayani humo. Muro amelazimika kukagua na kutoa elimu katika maeneo ya soko la Tengeru, USA River na Ngaramtoni baada ya kutoridhika na ugawaji wa vitambulisho hivyo, hali iliyopelekea uamuzi wa kuvigawa mwenyewe.
“Kweli nimechukia kuona wafanyabiashara wengi hawana elimu juu ya vitambulisho hivi, licha ya Rais Magufuli kuvizungumzia kila mara, ila watendaji wangu hawatoi elimu ili watu waelewe. Nimelazimika kuingia mitaani kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa utoaji vitambulisho hivi. Nimetoa maelekezo kwa wakurugenzi wa Halmashauri ya Arumeru na Arusha DC pamoja na maafisa tarafa na watendaji wa kata na vijiji kuacha tabia ya kuwasubiria wafanyabiashara maofisini na badala yake watoke na kuwafuata ili kuwapunguzia usumbufu wa kwenda umbali mrefu kuchukua vitambulisho hivi”. Ameeleza Mkuu wa Wilaya huyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa masoko ya Tengeru na USA River, Abia Mbise amesema kufuatia zoezi alilolifanya Mkuu wa Wilaya, itasaidia kuongeza mwitikio wa wafanyabiashara kupata vitambulisho kwa sababu hapo awali, walikuwa na mwitikio mdogo kutokana na changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo.