Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwita Waitara amesema serikali imepanga kufuta malimbikizo ya mikopo ya wanawake pamoja na vijana iliyotakiwa kutolewa kabla ya mwaka 2016, lakini Halmashauri zikashindwa kutoa fedha hizo kwa walengwa. Waitara amesema hayo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge Joram Hongoli wa Lupembe (CCM) aliyeuliza kwanini madeni hayo yasifutwe ili kuepuka mchakato wa ukaguzi kwenye Halmashauri husika.
Naibu Waziri huyo amesema hatua hiyo ni maelekezo yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) baada ya malimbikizo hayo kupelekea uwepo wa hoja za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Waitara amesema hivi sasa, uhakiki wa takwimu utakaoweka wazi kiasi kilicholimbikizwa katika Halmashauri nchi nzima unaendelea na mara baada ya zoezi hilo kufika tamati, taratibu za kufutwa malimbikizo hayo zitafanyika. Aidha, Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa TAMISEMI ipo bega kwa bega na Halmashauri ili kuhakikisha fedha za mikopo zinatolewa kama Sheria inavyoelekeza.
Mamlaka za serikali za mitaa kote nchini zimekuwa zikitoa asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.