Home FEDHA Tabia hizi zinakufilisi

Tabia hizi zinakufilisi

0 comment 120 views

Matumizi mazuri ya fedha ni changamoto kubwa kwa watu wengi kwani wengi hupata fedha na kabla hawajafanya mipango na fedha hizo, hujikuta wameishiwa, hali ambayo hupelekea mhusika kuanza kuhangaika ili aweze kujikimu. Muda mwingi suala huwa si kiasi cha fedha unachopata, mara nyingi matumizi na maamuzi ya fedha ndio husababisha watu wengi kushindwa kumudu kiasi cha fedha wanazopata na kujiwekea akiba kwa ajili ya mipango ya baadae.

Baadhi ya maamuzi ambayo husababisha watu wengi kushindwa kumudu na kujikuta hawana fedha kila wakati ni kama hizi hapa:

Malengo yanayokosa uhalisia. Hili ni tatizo kwa watu wengi kutokana na kuweka malengo makubwa ambayo mwisho wa siku inakuwa ngumu kutekeleza. Inapofika muda wa utekelezaji huwa tunabadilisha mawazo na kuelekeza fedha zetu katika mambo yasiyokuwa na umuhimu. Jitahidi kuweka malengo ambayo una uhakika wa kuyatekeleza ili kutumia fedha zako vizuri huku ukiwa na uhakika wa kesho. Anza kutekeleza malengo madogo ambayo yatakusaidia hapo mbeleni.

Kukosa bajeti. Kati ya vitu ambavyo watu wengi hupenda kupuuzia ni hili kuwa na ukomo wa matumizi. Utakuta mtu anaenda dukani kwa lengo la kununua nguo mbili lakini akifika anatamani viatu, pochi, saa na vitu vingine ambavyo hakupanga kununua. Kitendo hicho si kizuri kwa sababu nidhamu ya fedha huisha hivyo ni rahisi kupoteza fedha kwa muda mfupi kwa ajili ya mambo ambayo hayakupangwa. Jifunze kuandika mahitaji kabla ya kwenda kufanya manunuzi na jitahidi kununua vitu ulivyopanga kununua.

Mazoea ya kununua kwa bei rahisi. Wengi wana mazoea ya kununua vitu vya bei rahisi bila kutambua kwamba vitu hivyo mara nyingi sio imara na hivyo kusababisha kutumia fedha nyingi bila kujua. Ni vizuri kununua kitu kulingana na ubora na sio unafuu wa bei yake ili kuwa na uhakika wa kukitumia kwa muda mrefu.

Manunuzi ya vitu vilivyopo kwenye ‘sale’. Mara nyingi wafanyabiashara huuza bidhaa zao kwa bei rahisi zaidi hususani pale wanapokuwa wanataka kuleta mzigo mpya. Katika hili, wengi wanajikuta wakinunua vitu ambavyo hawavihitaji. Jifunze kununua vitu ambavyo una uhitaji navyo ili kupunguza matumizi mabaya ya fedha. Si kila kitu kinachouzwa bei nafuu lazima ununue, nunua bidhaa unazozihitaji na ambazo una uhakika wa kuzitumia.

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter