Kujiajiri ni ndoto ya kila mtu japokuwa sio kila mtu ana uwezo wa kuwa mjasiriamali au mfanyabiashara moja kwa moja. Kuna wale ambao wanaweza kufanya biashara na kuna wale ambao ni rahisi kuwa wawekezaji. Sababu mbalimbali humpelekea mtu kuanzisha biashara fulani, kwa mfano kupitia matatizo watu mbalimbali wameanzisha huduma na kuondoa tatizo huku wakijipatia kipato.
Kabla ya kufanya maamuzi yoyote muhimu kutafakari nia na madhumuni ya kutaka kuanzisha biashara husika. Hii itasaidia kuwa na mfumo endelevu wa biashara hiyo. Hata wafanyabiashara/wajasiriamali waliofanikiwa walijiwekea malengo wakati wanaanzisha shughuli zao.
Baadhi ya makosa ya kuepuka wakati unaanzisha biashara yako ni:
Kufanya kitu ambacho hukipendi
Imekuwa ni kawaida kwa waajiriwa kutowafurahia waajiri wao, jambo ambalo limewapelekea watu wengi kufikiria kufanya biashara na kujiajiri wenyewe. Ni muhimu wakati unavyotaka kuanzisha biashara kuwaza mawazo yatakayoifanya biashara hiyo izae matunda, iwasaidie watu wengine n.k hivyo basi kama maamuzi ya kufungua biashara yanatokana na mawazo binafsi ni tatizo kwani hakuna urahisi kwenye ajira za ofisini au ujasiriamali. Kabla hujaacha kazi uliyoajiriwa na kufikiria kuanza biashara tafakari kama biashara hiyo dio chaguo sahihi.
Kufanya kazi kwa muda mfupi
Ujasiriamali sio rahisi kama watu wanavyofikiria kwa sababu biashara ni ya kwako hivyo hakuna mtu wa kumlalamikia mambo yasipokwenda sawa. Vilevile ili biashara yako ilete mafanikio, unapaswa kufanya kazi mara mbili zaidi ya mtu aliyeajiriwa. Hivyo kama sababu yako ya kuanzisha biashara ni kupata muda wa kupumzika basi ni vyema ukajifikiria zaidi kwa sababu kujiajiri kunahitaji muda, kujituma na ubunifu.
Kutaka kufurahia maisha
Ni kweli kwamba ukiwa mjasiriamali unakuwa na uhuru wa kufanya mambo yako, kwa muda wako ili mradi shughuli zako zinaenda. Lakini unatakiwa kufahamu kuwa si kila wakati ni wa kufurahia maisha. Na kwa sababu huna muajiri, changamoto zote zinazoikabili biashara yako unatakiwa uzitafutie suluhu wewe na kufanikiwa au kushindikana kwa biashara yako hutokana na maamuzi yako hivyo inafaa kutambua kuwa kujiajiri ni jukumu kubwa zaidi.
Kutamani faida mapema
Kufanya ujasiriamali katika kitu unachokipenda ni muhimu sana, sawa suala la fedha ni muhimu kulitathmini lakini kwanza jiulize unataka ufungue biashara fulani kwa sababu ya fedha au kwa sababu unajua unaweza kuleta utofauti, kuleta suluhisho katika changamoto za kijamii n.k. Kama hauna mapenzi na biashara unayoifungua itakuwa ngumu kuimudu pindi matatizo yatakapotokea.
Rafiki au ndugu kutaka mshirikiane kufungua biashara
Biashara nyingi zimeshindwa kuendelea kwa sababu ya undugu na urafiki kwenye biashara. Si jambo jema sana kuanzisha biashara kwa sababu ndugu au rafiki amekushauri muanze biashara fulani. Badala ya kufanya hivyo, unaweza kumsaidia mtaji wenye riba nafuu kama yeye ndio ameleta wazo la biashara ili kuepusha matatizo.