Na Mwandishi wetu
Kampuni ya huduma za simu ya Vodacom imeorodheshwa rasmi kwenye Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE) jana Agosti 14 na imeweka sokoni jumla ya hisa zake bilioni 2.2. uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa soko la hisa akiwemo Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango.
Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Ian Ferrao amesema hatua hiyo ambayo ni maagizo ya serikali haikuja kirahisi, lakini walipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali hadi kufanikisha jambo hilo.
Waziri wa Fedha ambaye alikua mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za DSE ametoa pongezi kwa Vodacom na kuzitaka kampuni nyingine kuharakisha mchakato huu kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.
Mpango amesisitiza kuwa serikali itachukua hatua za kisheria kwa kampuni ambazo hazitatekeleza agizo hilo, pia amechukua nafasi hiyo kukumbusha kampuni hizo kushirikiana na wataalamu ya tasnia ya soko na mitaji kama Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) inavyoelekeza.