Wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga amewataka wahasibu na wakaguzi nchini kuhakikisha wanazingatia maadili ya kazi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya fedha haramu, ukwepaji kodi na malipo hewa ili kulinda taaluma zao na uchumi wa taifa.
Gavana Luoga ameeleza kuwa ikiwa wakaguzi na wahasibu nchini watatekeleza hayo basi watanzania watakuwa na imani nao hivyo kurahisisha kuondokana na changamoto kama malipo hewa na uingizwaji/uwepo wa fedha haramu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NBAA, Pius Maneno amesema mkutano huo wa siku tatu umelenga kujadili masuala mbalimbali yanayokabili sekta hiyo na kubadilishana uzoefu. Maneno ameongeza kuwa wanatarajia kujadili kuhusu fedha, Tehama, Uadilifu na Muongozo wa Wahasibu na Wakaguzi wa hesabu kuhusiana na fedha haramu pamoja na kanuni za nidhamu.
“Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu nchini imeendelea kuwaelimisha wahasibu na wakaguzi wa mahesabu juu ya kufanya kazi na kuzingatia wajibu na weledi pindi watekelezapo majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wale wote wanaokiuka maadili”. Amesema Mkurugenzi huyo.
Aidha, amesema kuwa tayari bodi hiyo imetunga mwongozo ambao umeanza kutumika tarehe 1 Aprili mwaka huu kwa wafanyabiashara wadogo ili kuhakikisha wanakagua fedha zao, lengo likiwa ni kuongeza kodi. Pamoja na hayo, amebainisha kuwa mwezi Mei mwaka huu wameanza kutumia mwongozo wa fedha haramu na Juni 15 mwaka huu wanategemea kuanza kutumia kanuni za uadilifu.
Mkutano huo umewashirikisha watu 300 ambao ni wahasibu na wakaguzi kutoka taasisi na mashirika mbalimbali nchini.