Home KILIMO Faida za kilimo cha Green House

Faida za kilimo cha Green House

0 comment 142 views

Green House (banda kitalu) ni mfumo wa kisasa wa kufanya kilimo ambao unasaidia mimea kukua vizuri na katika mazingira mazuri na salama. Kawaida, huwa kunakuwa na banda maalumu ambalo huwezesha mimea kukua licha ya mazingira na hali ya hewa kubadilika.

Mara nyingi wakulima hupata hasara ya mazao waliyopanda kutokana na mazingira haribifu yanayotokana na mvua kubwa, baridi, upepo mkali, joto kali, wadudu, magonjwa, pamoja na mionzi ya jua. Lakini kupitia tekinolojia ya Green house mkulima anakuwa na uhakika wa mimea yake kustawi bila kuathiriwa na mambo hayo.

Kwa Tanzania teknolojia hii bado ni ngeni kwa wakulima wengi, na wengi wao wanaona hakuna umuhimu wa kuifahamu kwa kuhofia gharama zake, jambo ambalo si kweli na ni vyema wakulima hasa wanaolima katika maeneo yenye baridi kali au joto kali kupewa elimu kuhusu aina hii ya kilimo hii ili kuongeza uzalishaji nchini.

Faida zake:

Kwa kutumia Green house mkulima anakuwa na uhuru wa kulima mazao mbalimbali, viungo, maua, nk. Na ana uwezo wa kubadilisha mazao anayolima kila mwaka au kuchanganya mazao hayo, kwa kufanya hivyo hata rutuba katika udongo huongezeka zaidi. Pia  Inaelezwa kuwa mazao hukua si chini ya mara kumi katika green house ukilinganisha na eneo la wazi.

Mkulima anakuwa na uhakika wa mavuno akitumia teknolojia ya green house kwa sababu mazao yake hayatoshambuliwa na uharibifu wa aina yoyote katika upande wa hali ya hewa na hata mazingira. Green house humhakikishia mkulima kuwa mazao yanakua katika hali ya hewa inayotakiwa, umwagiliaji unaotakiwa nk. Vilevile katika upande wa hali ya hewa na magonjwa mkulima akitumia green house anakuwa hana wasiwasi kuhusu masuala hayo.

Pia mkulima anayetumia teknolojia ya green house hupata fursa ya masoko kwani mara nyingi kila mazao mengi huwa na msimu wake, lakini kwa kupitia green house mkulima anaweza kuzalisha mazao ambayo yanahitajika zaidi kwa kipindi husika na kuyauza kwa bei nzuri katika masoko hivyo kuongeza mapato yake na ya nchi kwa ujumla.

Katika teknolojia ya green house si lazima mkulima atume udongo kupanda mazao yake. Hivyo mkulima anaweza kuepukana na changamoto ya wadudu na magonjwa yanayosababishwa na udongo. Aidha, ukiachana na suala la fedha ili kujipatia teknolojia hii, faida zake ni nyingi sana hivyo ikiwa mkulima anataka kupata maendeleo zaidi katika sekta hii basi anashauriwa kujiwekea akiba ambayo itamuwezesha kuipata teknolojia hii.

Kwa hapa nchini, kampuni ya Balton Tanzania ambayo ina makao makuu yake jijini Arusha ndio kampuni inayojishughulisha zaidi na kilimo cha green house.

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter